Lengo la mfugaji wa samaki ni vifaranga alivyovipandikiza bwawani vikue haraka ili viweze kufikia uzito unaotakiwa mapema inavyowezekana na, kwa hiyo, kuvunwa mapema kusudi kuokoa gharama za kuwatunza na kuwalisha kwa kipindi kirefu.
Ukuaji wa samaki bwawani huathiriwa na mambo kadhaa, makubwa yakiwa ni haya yafuatayo:
1. JOTO LA MAJI
Kila aina ya samaki inayofugwa bwawani ina mahitaji yake ya kiasi cha joto la maji. Kwa mfano, Sato (Nile Tilapia), hula vema na hukua kwa haraka maji yanapokuwa ni ya uvuguvugu. Ukitaka maji yabaki katika hali hii, chukua hatua zifuatazo:
(i) Wakati wote kina cha maji bwawani kiwe kati ya sentimita 30 na 100.
(ii) Wakati wote maji bwawani yawe yametulia. Kina cha maji kikishuka hadi sentimita 15, ongeza maji mapya.
(iii) Miti na mimea inayozunguka au inayokaribia bwawa na ambayo inazuia jua lisipige kwenye maji, ikatwe.
2. CHAKULA
Tofauti na samaki walio katika mito, maziwa na bahari, chakula cha kukuza samaki walio bwawani lazima kiwekwe humo na mfugaji mwenyewe. Katika mito, maziwa na bahari, vyakula vya asili vya aina mbalimbali hupatikana humo kwa kiasi cha kutosha. Hali ni tofauti katika bwawa ambapo eneo ni dogo na samaki huzaliana na kuongezeka haraka.
Kwa hiyo, mahitaji ya chakula ni makubwa kuliko upatikanaji humo wa vyakula vya asili. Ili samaki hao waweze kukua vizuri na haraka sharti vyakula viongezwe humo na mfugaji.
Unaweza kuongeza chakula bwawani kwa njia mbili zifuatazo:
• Kuongeza chakula cha asili bwawani kwa kurutubisha maji.
• Kuweka humo chakula cha ziada.
3. WINGI WA SAMAKI BWAWANI
Ili samaki wakue vizuri bwawani wanahitaji kuwa na nafasi ya kutosha. Samaki wakiwa wengi bwawani husongamana na kudumaa. Kudhibiti hali hiyo, chukua hatua zifuatazo:
• Kwa kila mita moja mraba, pandikiza vifaranga watano hadi saba kwa wanaozaliana na samaki 10 had 15 kwa wasiozaliana.
• Vua samaki mara kwa mara kwa kufuata ratiba au utaratibu maalumu.
• Maji yote yaondolewe bwawani kwa uvunaji wa mwisho kila baada ya miezi 6 hadi 12.
4. UMRI WA SAMAKI
Ukuaji wa samaki wadogo ni wa haraka kuliko wa samaki wakubwa (zaidi ya gramu 150 – 200). Kwa sababu hii, ili kupata mavuno makubwa kutoka kwenye bwawa lako fanya yafuatayo:
(i) Pandikiza samaki wadogo (visamaki) kwa sababu hukua haraka kuliko samaki wakubwa.
(ii) Mara samaki wakipata uzito unaotakiwa, ondoa maji yote bwawani, vuna samaki wote na baadaye pandikiza visamaki vingine.
5. UDHIBITI WA VISUMBUFU BWAWANI
Magonjwa na visumbufu vingine kama chura, kenge hudumaza samaki wanaokua.
No comments:
Post a Comment